Google+ simplisphoto: Tanzia: Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Moshi, Afariki Dunia

Translate

Thursday, February 7, 2013

Tanzia: Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Moshi, Afariki Dunia

Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie
Askofu mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki Moshi, Tanzania amefariki dunia Alhamisi, tarehe 7 Februari 2013 mjini Nairobi, Kenya alikokuwa akitibiwa saratani ya kibofu cha mkojo.

Kwa mujibu wa Radio Vatikani, habari za msiba zimethibitishwa na Askofu Isack Amani wa Jimbo Katoliki Moshi. Ibada ya mazishi itafanyika Alhamisi tarehe 14 Februari saa nne asubuhi katika Kanisa la Kristu Mfalme, Moshi.

Askofu Msarikie alizaliwa Kirua Vunjo Moshi, mwaka 1931. Alipewa daraja la Upadre tarehe 8 Agosti 1961 kama padre wa Jimbo la Moshi. Aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohani Paulo II kuwa askofu wa Jimbo la Moshi tarehere 21 Machi 1986. Alisimikwa rasmi kama askofu wa Jimbo la Moshi tarehe 1 Mei 1986 na Askofu Jozef Kadinali Tomko akisaidiwa na Makadinali Laurian Rugambwa na Maurice Michael Otunga.

Baada ya kulitumikia Kanisa la Moshi kwa miaka 26, Askofu Amedeus alistaafu kwa mujibu wa sheria ya Kanisa tarehe 21 Novemba 2007. Baada ya kustaafu, aliendelea kulihudumia kanisa kwa huduma mbali mbali za kiroho na kimwili. Jimbo la Moshi linaongozwa na Mh Askofu Isaac Amani Massawe tangu Novemba 2007.
Post a Comment