Tanzania kupitia Bodi ya Utalii Tanzania ilishiriki katika maonyesho ya Kimataifa ya Utalii yaliyofanyika mjini Paris, Ufaransa kuanzia Machi 21 na kuhitimishwa Jumapili Machi 24, 2013.
Katika banda la Tanzania, Bi Gloria Munhambo, Ofisa Mkuu wa Maelezo ya Utalii na Ofisa Mwandamizi wa Bodi ya Utalii Kanda ya Mwanza, akiongozana na maofisa wengine wa Bodi ya Utalii na Mamlaka ya Hifadhi za Wanyapori Tanzania (TANAPA) walikuwa na kazi kubwa ya kutangaza vivutio mbali mbali vya Tanzania kwa wageni waliotembelea banda la Tanzania.
Bi Munhambo alisema kuwa wageni wengi wametembelea banda la Tanzania. Wengi wa watu waliotembelea banda la Tanzania walionekana kuvutiwa na kupendelea kutembelea mbuga za wanyama, utalii wa kiutamaduni na kutembelea visiwa vya Zanzibar.
Kadiri ya Bi Munhambo, wageni wengi walikuwa wakiulizia upatikanaji wa usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Ufaransa kwenda Tanzania. Kwa sasa hakuna safari ya moja kwa moja, hivo watalii wanalazimika kutumia gharama kubwa ya fedha na muda kutokana na kukosekana kwa usafiri wa moja kwa moja. Bi Munhambo, alisisitiza kuwa kuwepo kwa Shirika la Taifa la Ndege fanisi lingeweza kuiongezea Tanzania watalii wengi zaidi na kuitangaza sekta ya Utalii.
Changamoto nyingine itakayofanyiwa kazi kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Ufaransa ni upatikanaji wa vipeperushi, video na nyaraka mbalimbali katika lugha ya Kifaransa ili kuwafikia Wafaransa wengi zaidi.
Katika banda la Tanzania yalishiriki pia makampuni yanayojihusisha na shughuli za kitalii kama vile Furahia Tanzania Safari et Trekking Ltd, na Tanganyika Expeditions.
|
Bi Manhumbo akiwa katika banda la Tanzania |
|
Picha ya pamoja ya Maofisa wa TANAPA, bodi ya utalii na makampuni binafsi walioshiriki katika maonesho ya Utalii |
|
Baadhi ya wageni wakijisomea vipeperushi vinavyoelezea vivutio vya Tanzania |
|
Bi Grace akimhudumia mteja katika banda ya bodi ya utalii Tanzania wakati wa maonesho |
Kwa picha zaidi bofya hapa:
Tanzania Katika Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii Paris
Commentaires