TANZIA: PADRE MICHAEL MASSAWE CSSp

Jumuiya ya Wamisionari na Watawa wa Shirika la Roho Mtakatifu wanasikitika kutangaza kifo cha mwanashirika mwenzao Padre Michael Massawe CSSp kilichotokea jumatatu tarehe 26 Octoba 2015 katika mji wa La Croix Valmer nchini Ufaransa.

Maziko

Maziko yatafanyika Ufaransa Ijumaa Novemba 6 saa nane na nusu mchana (saa za Paris sawa na saa kumi na nusu saa za Afrika Mashariki). Kwa desturi za wamisionari wa Roho Mtakatifu maziko hufanyika mahali alipofia.

Historia fupi

Padre Michael Massawe alizaliwa Septemba 29 mwaka 1960 katika kijiji cha Keni wilayani Rombo (Kilimanjaro). Aliweka nadhiri za kitawa Julai 6, 1988 katika novisia ya Magamba, Lushoto (Tanga). Alipewa daraja la Upadre tarehe 28 mwezi mei 1993 Usa River mjini Arusha.


Kama mmisionari, Padre Michael alitumwa kufanya kazi ya kimisionari nchini Congo Brazaville alikofanya kazi kati ya 1993-1999. Baadaye alirudi Tanzania na kufanya kazi kama mtunza  ‘bursar’ katika nyumba ya malezi ya Shirika la Roho Mtakatifu iliyoko Magamba wilayani Lushoto. Mwaka huo huo alitumwa kufanya kazi Ufaransa hadi 2002. Alilazimika kurudi Tanzania baada ya kuchaguliwa kama mshauri katika Uongozi wa Shirika kanda ya Afrika Mashariki. Alifanya kazi hiyo ya ushauri kwa miaka 6 hadi mwaka 2009. Wakati huo huo, alifanya pia kama mlezi wa wanovisi tangu 2002 hadi 2004. Kati ya 2006 na 2009 alifanya kazi Spiritan Center Bagamoyo. Alirudi Ufaransa mwaka 2009 hadi mauti yalipomkuta 2015. Akiwa Ufaransa alikuwa mlezi katika shule mjini Blotzheim na kama mkuu wa jumuiya 2010-2014. Kuanzia Novemba 2014 hadi 2015 alikuwa mkuu wa jumuiya ya Croix Valmer.

Kwa wale waliomfahamu, watamkumbuka kwa uchapakazi na ukarimu wake.

Mungu ampe pumziko la milele Padre Michael Massawe. Amina.

Commentaires

Posts les plus consultés de ce blog